Jumamosi, 16 Aprili 2016

MABASI YA KASI DAR KUANZA MEI 10


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amesema mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart), unatarajia kuanza rasmi Mei 10, mwaka huu. 


Akizungumza kwenye majumuisho ya ziara ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Simbachawene alisema baada ya kukutana na wadau wa mradi huo, wamewahakikishia kuwa utaanza rasmi mwezi ujao bila kukosa. 


“Tumeambiwa mradi huu una mikataba mingi na kuwa bado kuna mjadala mkubwa wa mikataba. Hatuwezi kulazimisha maana unaweza kujikuta ukitengeneza mikataba mibaya, hivyo tunaendelea na mijadala ya mikataba,” alisema. 


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza alisema wameutembelea mradi huo zaidi ya mara nne na kugundua tatizo linaloukwamisha kuwa ni fedha na kuitaka Serikali kutoa fedha ili uanze. 


Aliesema lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kupunguza kero ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanaokabiliwa na tatizo la usafiri na foleni za barabarani, hivyo kutumia muda mrefu barabarani. 


Rweikiza alisema kukamilika kwa mradi huo na kuanza kufanya kazi kutapunguza kero na kuokoa muda mwingi uliokuwa ukitumia bila uzalishaji.