Jumanne, 9 Juni 2015

Serikali imepunguza viwango vya tozo ya ardhi kwa asilimia 50 ya thamani ya ardhi kwa mashamba na viwanja.

Serikali imepunguza viwango vya tozo ya ardhi kwa asilimia 50 ya thamani ya ardhi husika kwa mashamba na viwanja kutoka asilimia kumi na tano ya sasa hadi asilimia saba nukta tano ya thamani ya ardhi ili kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kumudu kulipa kodi, tozo na ada za ardhi.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi kwa mwaka 2015/16, waziri wa ardhi Mhe. William Lukuvi amesema viwango hivyo vitaanza kutumika julai mosi mwaka huu na kusisitiza ada ya upimaji ardhi imepungua kwa asilimia 62.5 kutoka shilingi laki 8 hadi laki 3 kwa hekta. 
Akiwasilisha maoni ya kamati ya kudumu ya bunge ya ardhi maliasili na utalii, mwenyekiti wa kamati Mhe. James Lembeli amesema wawekezaji wamepewa maeneo makubwa ambayo hawayaendelezi na hivyo kuzusha migogoro na wananchi, huku kambi ya upinzani ikidai wamiliki wengi wa mashamba wanaikosesha serikali kwa kutolipa kodi ya ardhi.
Wakichangia maoni  ya bajeti ya wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi baadhi ya wabunge wameipongeza serikali kwa kufanikia kutatua migogoro ya ardhi kwa kurejesha mashamba yaliyovamiwa kwa wananchi pamoja na kupunguza tozo,ada na kodi mbalimbali za ardhi.