Jumamosi, 25 Juni 2016

SERIKALI YASITISHA KAULI YAKE YA CHAKULA HOSPITAL YA MUHIMBILI


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , imesitisha tamko la utoaji wa vyakula kwa wagonjwa watakaolazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kupisha utafiti wa kina kuhusu huduma hiyo ili kuweza kutoa kilicho bora kwa watanzania.


Akizungumza hayo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema kwamba wameamua kusitisha mpango mpaka watapotangaza tena ili kufanya utafiti kujua kama kuna faida au hasara kwa wananchi.


“Natoa tamko kwamba huduma hii iliyotarajiwa kuanza hivi karibuni isitishwe mara moja ili kupisha watafiti waweze kufanya uchunguzi kujua inawasaidia kwa kiasi gani wananchi”alisisitiza Bi. Mwalimu.


Aidha Bi. Mwalimu amesema kwamba huduma hiyo itatolewa kwa wagonjwa watakaolazwa hapo kwa kulipia shilingi elfu 50 ikiwemo shilingi elfu kumi ya kumuona daktari , elfu kumi ya kitanda na elfu 30 iliyobaki ni kwa malipo ya chakula kwa wiki.


“Huduma hii inalenga kuwasaidia wananchi katika kuwaandalia chakula stahiki kwa wagonjwa na kupunguza usumbufu kwa waangalizi wa wagonjwa wao kuleta vyakula hospitalini ili kuimalisha afya zao kwa ujumla”aliongeza Bi.Mwalimu.

Alhamisi, 16 Juni 2016

POLISI YAVAMIA NYUMBA YA GWAJIMA


Taarifa zilizotufikia muda huu zinasema Polisi 6 wakiwa ndani ya Landcruiser wamezingira nyumbani kwa Askofu Josephat Gwajima. 


Sababu za kufanya hivyo bado hazijafahamika, tutaendelea kuwajuza kadri tunavyoendelea kupata taarifa.

WATANZANIA ASILIMIA 100 WANATAKA BUNGE LIONESHWE LIVE


TAASISI ya Twaweza imetoa matokeo ya utafiti wake, ambapo imebainika kuwa asilimia 79 ya Watanzania wamepinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja (Live ) ya Bunge.


Katika maoni yao, wananchi hao wamedai kuwa ni haki yao ya msingi kufahamu kinachoendelea katika vikao mbalimbali vya Bunge.


Utafiti wa taasisi hiyo umefanywa katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara kupitia mpango wake wa Sauti za Wananchi.


Akitoa taarifa ya matokeo ya utafiti huo jana jijini Dar e Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze,  alisema suala hilo limeonekana kutokuungwa mkono na wananchi wengi.


“Asilimia kubwa ya Watanzania wanapinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge. Suala hili limeonekana kugusa hisia za watu wengi na maamuzi haya ya Serikali yakionekana kutoungwa mkono.


“Katika utafiti huu wananchi nane kati ya 10 wanapinga uamuzi wa hali inayodhihirisha kutoungwa mkono kwa hatua hiyo,” alisema Eiyakuze.


Akizungumzia sababu walizozitoa  wananchi wanaotaka matangazo ya Bunge yarushwe moja kwa moja,  Eiyakuze alisema asilimia 46 walisema yanawafanya waweze kufuatilia utendaji wa wabunge waliowachagua kwa kuwa huko ndio walikowatuma.


“Asilimia 44 wanasema ni muhimu kwa sababu wananchi wanahaki ya kufahamu kinachoendelea bungeni, asilimia 29 wanasema matangazo ya moja kwa moja yalikuwa yanaaminika zaidi kwa watazamaji na wasikilizaji  kuona na kusikia wenyewe kile kinachoendelea tofauti na mfumo wa kurekodi ambapo kuna baadhi ya mambo yanahaririwa.


“Asilimia 16 walidai kuwa inafursa mwananchi kupata taarifa sahihi badala ya kuzisoma kwenye magazeti huku asilimia 16 nyingine wakisema inawasaidia wanachi kufuatilia mijadala ya Bunge kwa wakati”, alisema Eiyakuze.


Pamoja na hali hiyo mkurugenzi huyo alisema katika utafiti huo asilimia 92  ya wananchi walisema kuna umuhimu wa vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa moja kupitia Luninga na redio bila kujali gharama zilizoelezwa kuwa ndio chanzo cha kufikia uamuzi huo.


“Asilimia 88 walisema vipindi vya Bunge virushwe ‘Live’ bila kujali gharama ukilinganisha na asilimia 12 ambao waliona ni muhimu suala la bajeti likazingatiwa,” alisema.


Mkurugenzi huyo alisema asilimia 80 wanaona matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni ni muhimu kama yalivyo na asilimia 20 wakisema fedha hizo zitumike kwenye huduma nyinge za jamii.


Akizungumzia suala la vyombo vya habari vya binafsi kuruhusiwa kurusha matangazo hayo,  Eiyakuze alisema wananchi wanaunga mkono vyombo hivyo kuruhusiwa iwapo Serikali imeshindwa kumudu gharama.


Utafiti huo pia umeonesha Watanzinia wanne kati ya kumi wamewahi kuangalia matangazo ya moja kwa moja kupitia Luninga na sita kati ya kumi  wamesikiliza kupitia redio.


Aidha utafiti huo umeonyesha zaidi ya nusu ya wananchi walosema wameangalia au kusikiliza vipindi vya Bunge wamefanya hivyo ndani ya miezi miwili iliyopita.


Hali ilivyokuwa

Januari mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Nape Nnauye, alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hatua ya Serikali kusitisha matangazo hayo kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).


Miongoni mwa sababu alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama kubwa ya Sh bilioni 4.2 zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya moja kwa moja kwa mwaka pia watumishi wa serikali kushabikia Bunge badala ya kuendelea na kazi ofisini.


Hatua ya Serikali kusitisha matangazo hayo iliibua mjadala mkubwa bungeni huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, (ACT-Wazalendo) akilitaka Bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili taarifa hiyo ya Serikali.


Siku chache baadaye kilio hicho cha ukosefu wa fedha za kuonesha matangazo hayo ya moja kwa moja ambacho kimekuwa kikitolewa na serikali, sasa kilipata ufumbuzi.


Hatua hiyo iliyokana na uamuzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF), kujitokeza hadharani na kueleza kwamba upo tayari kutoa fedha zinazohitajika ili kuhakikisha haki ya Mtanzania kupata habari kupitia TBC haiingiliwi wala kubughudhiwa kwa hoja yoyote.


Endapo Serikali itakubali ombi hilo, wananchi wataendelea kunufaika na vikao vya moja kwa moja vya Bunge tofauti na pendekezo la serikali la kunakili baadhi ya sehemu na kisha kuoneshwa usiku.

Jumatano, 15 Juni 2016

SIMU FEKI KUZIMWA RASMI KESHO




SIMU ziliingizwa nchini zikiwa hazina kiwango kuzimwa rasmi kesho, katika kuhakikisha kila mtu anatumia simu kiwango kwa usalama  na ulinzi wa nchi.


Akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Mhandisi James Kilaba amesema kuwa katika uzimaji wa simu wameshatoa elimu juu ya simu hizo.


Kilaba amesema kuwa simu ambazo watu walibadilisha (Flash) nazo zitazimwa kutokana na kufanya hivyo ni kosa la kisheria na mtu anayefanya hivyo kifungo chake ni miaka 10.


Amesema hakuna kitu chochote kinachofanya simu zisiweze kuzimwa hivyo watu wajiandae kwa zoezi hilo na simu zitakazozimwa wametakiwa kuzihifadhi katika mazingira salama.


Aidha amesema wametoa elimu ya kutosha, hivyo kesho kutakuwa na mkutano wa wadau mbalimbali wa makampuni ya simu, na wamiliki wa maduka ya simu pamoja na mafundi katika kubadilishana mawazo wakati wa kuzima simu feki.


‘’Simu feki kesho zitazimwa, hatutakuwa na mabadiliko ya kuongeza muda au vinginevyo kutokana na elimu iliyotolewa juu ya simu ya  feki ambazo baada ya soko kushindikana mjini walipeleka vijijini’’amesema Kilaba  .

Jumanne, 14 Juni 2016

Lipumba wamkataa cuf


Wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitengua uamuzi wake wa kung’atuka kwenye wadhifa huo na kuomba kurejea, viongozi wa juu wa chama hicho wamepinga hatua hiyo wakisema katiba yao hairuhusu na kwamba anakwenda kukiua chama.


Kauli za viongozi hao, zimekuja muda mfupi baada ya Profesa Lipumba kutangaza nia hiyo jana kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni huku akibainisha kuwa amefanya hivyo baada ya kuombwa.


Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Lipumba hawezi kuwa na nia njema ya kukijenga chama hicho endapo atarudishwa kwenye nafasi aliyoikataa.


“Anataka kuja kukiharibu chama,” alisema Mazrui. Alifafanua kuwa tayari chama hicho kimefanya mambo mengi bila Lipumba ambaye alikuwa anaona kila kinachoendelea, hivyo alichokisema hakina mashiko kwani CUF ilisharidhia kuitisha mkutano wa uchaguzi kujaza hiyo.


Akieleza sababu alizozitoa mwenyekiti huyo, Mazrui alisema haoni chochote cha maana. “Sababu zilizomuondoa zingalipo. Kinachomrudisha ni nini?”alihoji naibu katibu mkuu huyo.


 Alisisitiza kuwa Wazanzibari wanaendelea na mchakato wa kuidai haki yao iliyoporwa Oktoba 25 na hawana nafasi ya kushughulika na masuala yasiyokuwa na tija kwao, hivyo haoni kama kuna sababu ya kumjadili Lipumba na nafasi yake badala ya kuendelea pale walipo.


 “CCM wanaona kinachoendelea, hivyo wameona wamtumie Lipumba kuja kuharibu mipango yetu. Hatuna muda wa kumjadili.Tunataka haki iliyoporwa,”alisisitiza. 


Msimamo wa Mazrui haukutofautiana sana na ule wa Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Twaha Taslima aliyebainisha kuwa amesikia taarifa za kurudi kwa Profesa Lipumba, lakini haoni uwezekano huo. 


“Katiba hairuhusu hilo.Hakuna kifungu kinachotoa nafasi kwa kiongozi aliyejiuzulu kurudi kwenye nafasi yake pindi atakapotaka kufanya hivyo,” alisema Taslima.


Aliielezea Ibara ya 117 (2) iliyotumiwa na Profesa huyo kuandika barua ya kutengua uamuzi wake, kuwa inatoa tafsiri zaidi ya moja hivyo kuwapo haja ya viongozi kukutana na kujadili suala hilo kabla ya kutoa maamuzi.


Kwa kuwa hakuwapo kwenye mkutano huo, Taslima alisema: “Tunahitaji kukutana haraka na kujadili. Tutafanya mkutano wetu na tutavijulisha vyombo vya habari ndani ya wiki hii.”


Taslima alisema kipindi alichoongoza kilikuwa na changamoto nyingi ambazo ni tofauti na sasa, hivyo haoni haja ya mtu mwingine kuja wakati mambo yametulia. Chama hicho kilipanga kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo Agosti mwaka huu.


Baada ya kung’atuka kwa Lipumba, Taslima alichukua mikoba yake na kukivusha chama hicho kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, pamoja na ule wa Zanzibar ambao uliahirishwa na chama hicho kususia marudio yake Machi 20 mwaka huu.


Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya alisema upo uwezekano wa Lipumba kurudi kwenye nafasi yake kwasababu mpaka sasa haijazibwa.


“Mwenyekiti huchaguliwa au kutenguliwa na halmashauri kuu. Haikupitisha kujizulu. Barua ya kujiuzulu itaenda pamoja na hii ya kutengua uamuzi wa awali,” alisema Kambaya.


Kauli ya Lipumba 

Awali, Profesa Lipumba alisema mara kadhaa amekutana na viongozi wa dini na chama pamoja na wanachama wa CUF na wote walikuwa na ujumbe mmoja tu…’rudi tukijenge chama.’ 


Profesa Lipumba hakushiriki mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambao kwa upande wa Zanzibar, kutokana na hitilafu zilizojitokeza ulifutwa na kurejewa Machi 20 mwaka huu huku chama hicho kikiwa kimesusia marudio hayo. 


Pamoja na hayo yote, Lipumba alisema ametafakari sana juu ya hali ya kisiasa Zanzibar na kuona umuhimu wa kutoa ushirikiano ili mambo yaende kwa manufaa ya taifa. 


“Ni lazima nchi iendeshwe kwa misingi ya demokrasia ambayo itapatikana kwa umoja wetu.Nimerudi kushirikiana na wenzangu kutimiza malengo hayo ili kuchangia maendeleo ya Tanzania,”alisema Profesa Lipumba. 


Lipumba aliachana na uongozi wa chama hicho, Agosti 8, mwaka jana, siku chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa kukubaliana kumsimamisha Edward Lowassa.


Alimuandikia barua Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad kuwa hakubaliani na uamuzi wa chama chake kuridhia makada waliohama Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Lowassa, kupewa fursa ya kugombea nafasi za uongozi.


Baada ya kukatwa kwenye mchujo wa ndani ya CCM, Lowassa akiwa na makada kadhaa wa chama hicho akiwamo aliyewahi kuwa waziri mkuu, Frederick Sumaye, alihamia Chadema ambako alipewa fursa ya kupeperusha bendera ya chama hicho kilichomo ndani ya Ukawa.


Lipumba hakukubaliana na hilo, alikaa pembeni na kuachia ngazi ingawa alishiriki tukio la kumkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa.


Jana, wakati anatangaza kufanya mabadiliko ya kile alichokiamua miezi 10 iliyopita, hakuruhusu maswali, ila alifafanua kile kitakachofuata baada ya kuwasilisha ombi hilo, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho: “Katibu Mkuu anashauriana na wanasheria kabla suala langu halijapelekwa kwenye halmashauri kuu kama katiba inavyosema,” alisema Profesa Lipumba.

KADA WA CCM CHARLES MWAKIPESILE AWASHANGAA WAPINZANI

Jumatatu, 13 Juni 2016

CHEKA KIDOGO NA VITUKO VYA JOTI

UVCCM MKOA WA MBEYA NA SONGWE WATOA TAMKO LA KUMUUNGA MKONO NAIBU SPIKA DR. TULIA ACKSON


Mwenyekiti wa Uvccm mkoa wa mbeya na songwe Aman kajuna ametoa tamko la Umoja wa vijana (UVCCM) la kumuunga mkono mh. Dr. Tulia Akson Naibu spika wa bunge la jamuhuri ya muungano wa tanzania .Akisoma risala mbele ya waandishi wa habari alisema wanasikitishwa na kulaani vikali na vitendo vinavyofanywa na wabunge wa upinzani vya kutaka kumhujumu naibu spika kwa sababu zao binafsi zisizo na maslahi kwa umma isipokuwa kwa vyama vyao pekee kwani uwezi kumuondoa naibu spika kwa kusimamia kanuni na taratibu zilizotungwa na wao wenyewe waheshimiwa wabunge na kuwanyima wananchi waliowachagua .Rai yao kwa wapinzani Wanawashauri wapinzani kurejea maneno ya busara yaliyotolewa na Dr. Harrison Mwakyembe. UVCCM imewaomba wabunge wa upinzani walejee bungeni kuwawakilisha wananchi waliowachagua kwa kuwatetea kwa hoja za msingi zenye maslahi kwa taifa na sio vyama vyao Pekee.

MASHINDANO YA KIMONDO CUP YAFUNGULIWA RASMI


Mashindano ya Kimondo Cup hatimaye yamezinduliwa siku ya Jana katika uwanja wa mlangali wilayani mbozi Mkoa wa Songwe. Akitoa risala fupi Mh. Diwani wa kata ya mlangali ambaye pia ni Mwenyekiti wa halimashauri ya Mbozi Erick Ambakisye alisema mashindano hayo yamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo uendeshaji wake umekuwa mgumu Sana ukizingatia mashindano hayo hayana mdhamini.lakini pia alisema faida ya mashindano hayo yameonekana kwa kipindi kilichopita cha miaka miwili kwa kutoa wachezaji kwenda ligi kuu .akiwemo Geofrey mwashiuya anaikipiga timu ya yanga na Geofrey mlawa anaekipiga mbeya city. Naye mgeni rasmi wa ufunguzi wa kimondo cup mkuu wa wilaya ya mbozi mkoa wa songwe mh.Ahmad alisema kwa upande wa serikali itashirikiana kuwasaidia kujenga mahusiano na makampuni ili waweze kudhamini mashindano hayo.

Pamoja na hayo ulipigwa mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo Kati ya mabingwa watetezi wa msimu uliopita wembe fc waliofanikiwa kushinda mchezo huo kwa magoli 2 kwa 1 dhidi ya haterere fc mashindano haya yanatarajia kuanza kesho katika viwanja mbalimbali wilayani mbozi Kata ya mlangali.

Mabingwa watetezi wa Kimondo Cup Wembe Fc wakiwa katika picha ya pamoja kabla  mchezo kuanza wa ufunguzi.